Jumatatu , 9th Aug , 2021

Serikali mkoani Arusha imesema kuwa itatoa kifuta machozi kwa familia zote za watoto watatu waliofariki dunia baada kushambuliwa na kundi la Simba katika Kijiji cha Ngoile wilayani Ngorongoro usiku wa Agosti 3, 2021.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro, Juma Muhina

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro, Juma Muhina, na kusema kwamba tayari serikali wilayani humo imeandaa utaratibu mzuri wa kufuta machozi kwa kila familia zilizofikwa na misiba ya watoto hao.

Siku ya tukio ilidaiwa kwamba watoto hao ambao walikuwa ni wanafunzi wa shule ya msingi Ngoile, walifikwa na mauti hayo mjira saa 4:00 usiku wakati wakitafuta mifugo yao iliyokuwa imepotea.

Serikali imeendelea kutoa wito kwa jamii za kifugaji zinazoishi karibu na hifadhi, kuchukua tahadhari kwa watoto pale wanapowapa majukumu ya kuchunga mifugo.