Jumatano , 26th Mei , 2021

Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Mrisho Mashaka Gambo, amelitaja zoezi la urasimishaji wa makazi kama zoezi lililojaa kichefuchefu kutokana na zoezi hilo kutokukamilika kwa mwaka sasa licha ya wananchi kutoa fedha zao.

Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Mrisho Mashaka Gambo,

Mhe. Gambo ameeleza hayo Bungeni wakati akichangia hoja kwenye majadiliano ya bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambapo amesema suala la urasimishaji litampunguzia Waziri Mhe. William Lukuvi umaarufu kwa wananchi.

“Kama kuna zoezi ni kichefuchefu ni urasimishaji, tuna kata nyingi katika Jiji la Arusha ambazo watu wamekwenda kufanya zoezi la kurasimisha, wamechukua fedha za watu na zoezi halijakamilika zaidi ya mwaka mambo haya hayaendani na serikali,” amesema Mhe. Gambo.

Awali akielezea juu ya migogoro ya ardhi na uwepo wa mashamba yasiyoendelezwa Mhe. Gambo amesema bado kuna kigugumizi katika suala hilo hususan katika Jiji la Arusha.

“Shida hii nchi kuna double standard kuna maeneo mengine maamuzi yanafanyika haraka, maeneo mengine kuangalia maslahi ya nchi, maeneo mengine kuna kuchelewa, yako mashamba ambayo hayajaendelezwa kwenye nchi serikali imeshayachukua, lakini kwa upande wa Jiji la Arusha kuna kigugumizi kikubwa sana,” amesema Mhe. Gambo.

Naye Mbunge wa Jimbo la kondoa Mjini Mhe. Ally Makoa akitoa hoja yake ameiomba serikali kuliangali suala zima la utoaji hati ikibidi wananchi wauziwe hati na si maeneo.

“Tuweke mfumo rahisi wananchi kupata hati mapema ikiwezekana wananchi wauziwe hati na sio wauziwe maeneo, maandalizi ya hati yatangulie alafu watu watangaziwe kuuziwa viwanja ambavyo vimekamilika hati,” amesema Mbunge Makoa.