Jumamosi , 7th Nov , 2020

Chifu Mkuu wa kabila la Unyanyembe Chifu Msagata Ngulati Said Fundikira, amesema kuwa upo umuhimu mkubwa wa wanawake kupewa nafasi ya kuongoza kwa kuwa upo mfano wa waliopewa fursa hiyo na wanafanya vizuri katika nafasi za uongozi.

Chifu Mkuu wa kabila la Unyanyembe Chifu Msagata Ngulati Said Fundikira.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Novemba 7, 2020, kwenye kipindi cha SupaBreakfast ya East Africa Radio, wakati akizungumzia na kutoa ushauri kwa wanaume kuwa wawe mstari wa mbele kwa ajili ya kuwaelimisha wanawake kutambua haki zao na kwamba wanayo fursa ya kuongoza kama wakipewa nafasi.

"Suala kubwa ambalo tunapaswa kufanya sisi kama wanaume kwa sababu tumeathirika sana na huu mfumo dume, kwahiyo tunahitaji tupate elimu ya kutosha na pia kuwapa ujasiri wakinamama wajue na wao wana uwezo mkubwa wa kuongoza", amesema Chifu Fundikila.

Adha Chifu Fundikila ameongeza kuwa, "Wanawake ni binadamu kama walivyo wanaume, wana akili, wana uwezo wa kufikiri na kupanga mambo ya maendeleo kwa jamii yao na hata jamii nyingine hivyo tuwape nafasi".