Alhamisi , 24th Sep , 2020

Ofisa Mtendaji Mkuu, wa klabu ya Simba SC Barbara Gonzalez amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika CAF, Ahmad Ahmad kwenye makao makuu ya shirikisho hilo yaliyopo jijini Cairo nchini Misri.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC Barbara Gonzalez wa pili kulia akiwa kwenye mazungumzo na Rais wa Shirikisho la soka barani Afrika CAF Ahmad Ahmad wa pili kutoka upande wa kulia

Barbara amekutana na Rais Ahmad, alipofanya ziara kwenye makao makuu ya Shirikisho hilo ikiwa ni muendelezo wa ziara za Afisa mtendaji huyo ambapo siku chache zilizopita alifanya ziara katika klabu ya Al Ahly na Zamaleki zote za nchini Misri pia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na klabu ya Simba kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Rais huyo wa CAF, amempongeza Barbara kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo kubwa kwa ngazi ya klabu huku akimtaka kuitumia vema fursa hiyo ili awe mfano kwa wanawake wengine.

Wengine waliohudhuria kikao hicho ni Katibu Mkuu wa CAF, Abdelmounaïm Bah, Makamu Katibu Mkuu wa CAF, Anthony Baffoe na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Mulamu Nghambi.

Huu ni muendelezo wa ziara kwa Afisa Mtendaji Mku wa Simba nchini Misri ambae ameongozana na Mjumbe wa Bodi ya wakurugenzi wa klabu hiyo Mulamu Nghambi, kwani siku chache zilizopita walifanya ziara makao makuu ya klabu ya Al Ahly yaliyopo jijini Cairo, Misri na kukubalina kushirikiana kwenye maeneo ya biashara, ufundi na uendelezaji wa wachezaji kwa kujenga kituo cha kukuza vipaji.

lakini pia viongozi hao wa Simba walitembelea makao makuu ya klabu ya Zamalek na walipata nafasi ya kukutana na viongozi wa klabu hiyo na wamekubaliana kushirikiana katika mambo mbalimbali ambayo yataisaidia klabu ya Simba kupiga hatua