Jumatano , 23rd Sep , 2020

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nhini James Kaji amepokea vitakasa mikono kutoka Umoja wa Nchi za Ulaya kupitia Mradi wa EU-ACT ambapo wametoa mashine 12 za kunawia mikono pamoja na sabuni zake kwa vituo vya kulea waathirika wa dawa za kulevya.

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nhini James Kaji akipokea taulo za kike aina ya Lavy Pads kutoka kwa Mwanamitindo Flavian Matata (kulia).

Sanjari na vitakasa mikono hivyo kwa ajili ya kujikinga na magonjwa ya kuambukiza amepokea pia taulo za kike aina ya Lavy Pads kutoka kwa Mwanamitindo wa Kimataifa Mtanzania Flavian Matata kutokana na kuwa na changamoto ya ukosefu wa taulo hizo katika baadhi ya vituo.

Akizungumza baada ya kupokea misaada hiyo na kuikabidhi kwa walengwa Jenerali Kaji amesema kuwa, Mamlaka haipambani tu na uingizwaji wa madawa nchini lakini pia inatoa Elimu kwa ambao tayari wameathirika na madawa hayo na kuhakikisha wanarudi katika hali za awali.

"Hatuishii katika kupambana na wauzaji pekee, tunatoa elimu kwa jamii kutojiingiza katika biashara hiyo haramu na utumiaji pia, tunahakikisha vituo vya kulea waathirika wa dawa za kulevya nchini (Sober houses) vinakuwa msaada kwa waathirika wa madawa ya kulevya ili kuokoa nguvu kazi ya Taifa", amesema Jenerali Kaji.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo mmoja ya waanzilishi wa vituo vya kulea waathirika wa dawa za kulevya, Nuru Ahmed amesema kuwa wadau wajitokeze kuwatembelea maana wanawake wengi wakiwa kule hawawezi kujitengenezea kipato kwahiyo huwa na changamoto ya mahitaji.