Jumatatu , 3rd Aug , 2020

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo ametangaza rasmi leo Agosti 3 kila ifikapo mwezi Agosti tarehe 3, 4 na 5 za mwezi huo zitakuwa siku maalumu za kuadhimisha 'TAMISEMI DAY'.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo

Amesema hayo Mkoani Dodoma akiwa anaongea na waandishi na watendaji baada ya  kufanya mazoezi wakiadhimisha siku ya afya, ambapo alisema kila itapofika mwezi Agosti kwa miaka yoyote kuanzia tarehe 3 hadi tarehe 5 za mwezi huo siku hizo zitaitwa 'TAMISEMI DAY'.

 “Leo hii TAMISEMI ambapo tumeamua tuwe na siku maalumu inaitwa 'TAMISEMI Day' lakini ndani yake tumeunganisha vitu vitatu, kutakuwa na siku tatu mfululizo ambapo siku ya kwanza itakuwa siku ya Afya , Siku ya pili itakuwa ya Elimu na siku ya tatu ni siku ya miundombinu", amesema.

Aidha Jafo amesema siku hizo watazitumia kueleza mambo aliyoyafanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli katika sekta ya afya, sekta ya elimu na sekta ya miundombinu ili kuwapa wananchi mrejesho wa kiutendaji.

Selemani Jafo alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kutokana na kuwa na maono mapana sana ambayo yamesaidia kuboresha sekta ya afya nchini hasa kwa upande wa vijijini ambapo baadhi ya wananchi walishakata tamaa kufikiwa na huduma hizo.