Jumamosi , 9th Mar , 2019

Mapema leo Mamia ya wakazi wa wilaya ya Monduli mkoani Arusha walikusanyika uwanja mdogo wa Arusha kumsubiri Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye amerejea Chama cha Mapinduzi (CCM).

Edward Lowassa akiwa na mwanaye Fred Lowassa.

Watu hao wakiwepo familia ya Lowassa, wakiongozwa na mtoto wake, Fred Lowassa wamesema wamerejea nyumbani CCM na Lowassa.

Fred ambaye naye alijiunga na CHADEMA baada ya baba yake kutimkia CHADEMA Julai 28, 2015, amesema familia yote ya Lowassa imerejea nyumbani CCM.

"Kama alivyosema mzee amerudi nyumbani na sisi kama familia tumerudi kumuunga mkono" amesema Fred.

Amesema anajisikia vizuri kurudi nyumbani kuendelea kushirikiana na rafiki zake ambao aliwaacha CCM na ambao bado wapo CHADEMA.

Lowassa aliyetimkia CHADEMA akitokea CCM ambako alipitishwa kugombea Urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Machi 1, 2019 alitangaza kurudi CCM na leo Jumamosi Machi 9, 2019 amerejea nyumbani kwake, Monduli mkoani Arusha.