
Tatizo hilo limetolewa ufafanuzi wa kisheria leo kutoka kwa Mwanasheria, Emmanuel Lukashu kupitia kipindi cha SUPA MIX kinachorushwa na East Africa Radio ambapo amesema.
“ Ni kosa la jinai kwa mujibu wa kanuni ya adhabu, sura ya 16 ya mwaka 2002 ambayo katika kifungu cha 139 kimeainisha wazi kwamba ni kosa kwa mtu yoyote anayenufaika kwa ngono au kufanya jambo lolote linaloashiria kujinufaisha kupitia shughuli hiyo “.
Mwanasheria huyo pia amevichambua vifungu hivyo kuanzia kifungu cha 139, kifungu cha kwanza (a) kinaongelea mazingira ambayo binti katika umri wowote ule ambaye ameamua mwenyewe ama kwa kulazimishwa, anaishi Tanzania au nje ya nchi, ni kosa kisheria kufanya shughuli hiyo. Katika kifungu cha 139(b) pia kinaeleza kuwa ni kosa kwa binti chini ya miaka 18 ambaye ni mtanzania ama kutoka nje ya nchi akiwa amelazimshwa ama kwa matakwa yake kufanya shughuli hiyo.
Lakini pia sheria hiyo inawagusa wanaume ambao aidha wapo chini ya miaka 18 ama zaidi, raia wa Tanzania au kutoka nje ya nchi kujishughlisha na vitendo vya kujinufaisha kwa kununua ama kununuliwa kwaajili ya ngono.
Kwenye upande wa adhabu, sheria inawahukumu pande zote mbili, upande wa mwanaume anayekwenda kununua na mwanamke anayenunuliwa au mwanamke ambaye amemshawishi mwanaume kununua, ambapo wanahukumiwa kifungo cha kuanzia miaka 10 hadi 20 au kulipa faini ya kuanzia laki moja hadi laki tatu au vyote kwa pamoja.