Ijumaa , 20th Jun , 2014

Serikali ya Tanzania inaendelea kutekeleza mpango wake wa ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika kila wilaya nchini hasa wilaya ambazo hazina kabisa chuo cha aina hiyo na maeneo yenye miradi mikubwa ya kitaifa kwa manufaa ya watanzania.

Naibu waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi Bi. Jennister Mhagama.

Naibu Waziri wa Elimu na Ufundi stadi Jennister Mhagama amesema amesema hayo wakati akijibu swali la Mhe. Deo Fikunjombe aliyetaka kufahamu ni lini serikali itatekeleza ahadi ya kujenga chuo cha Ufundi stadi Ludewa Shauri Moyo.

Kwa mujibu wa naibu waziri Mhagama, serikali imekwishaanza mchakato wa kutekeleza mpango huo kwa kutafuta washauri elekezi katika kila wilaya na ujenzi utaanza mapema mwezi ujao baada ya kuidhinishwa kwa bajeti kuu ya Serikali.

Wakati huohuo, taasisi ya sayansi ya habari na mawasiliano nchini Tanzania TEHAMA, imewataka waandishi wa habari kutumia teknolojia mpya ya kuwasilisha habari kwa maendeleo ya taifa.

Akizungumza jijini Dar-es-salaam katika kongamano lililoandaliwa na shule kuu ya uandishi wa Habari, Mkurugenzi wa Tehama Dkt. Joseph kilongola, amesema kwa sasa mitandao mingi ya habari inakiuka maadili kwa kuweka habari zisizo na maadili kwa jamii.

Kihongola ameongeza kuwa TEHAMA kwa sasa inashughulikia mitandao yote ya habari hususani mablogu na kuzuia habari zote zisizokuwa na manufaa kwa jamiii.