
Wakipatiwa huduma ya kwanza mara baada ya kuokolewa
Tukio hilo lilitokea siku ya Jumatano ya wiki iliyopita ambapo jitihada za kuwaokoa zilikuwa zikifanyika kwa takriban siku 4 mfululizo hadi siku ya jana ambapo waokoaji walifanikiwa kucharanga mwamba na kupata upenyo uliowezesha mawasiliano kati ya waokoaji, na watu hao.
Zoezi limekamilika leo majira ya saa 5:02 asubuhi na kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita kwa ajili ya uchunguzi zaidi baada ya kupatiwa huduma ya kwanza
Kwa mujibu wa taarifa kutoka mkoani Geita, wachimbaji hao wameokolewa ikiwa ni ndani ya saa 24 tangu walipojibu ujumbe uliotumwa kwao, na wao wakajibu wako hai na wanachohitaji ni kupelekewa chakula,
Taarifa zaidi zinasema, mchimbaji wa kwanza alkokolewa majira ya saa tatu leo asubuhi na kufuatiwa na wenzake, walioonekana wakiwa wamejaa tope lakini wakiwa na afya njema. Wachimbaji hao ni Watanzania 14 na raia mmoja wa China.
Zoezi la kuwaokoa lilishuhudiwa na Naibu Waziri wa Nishati Madini, Dk. Medard Kalemani pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja Jenerali Ezekiel Kyunga.
Uchunguzi wa nini hasa kilisababisha ajali hiyo unaendelea, lakini hii si mara ya kwanza kwa tukio kama hili kutokea
Novemba, mwaka 2015 wachimbaji watano waliokolewa wakiwa hai baada ya kukwama chini ya ardhi kwa siku 41 katika mgodi wa dhahabu wa Nyangalala mkoani Shinyanga .
Mara baada ya zoezi hilo kukamilika, watu pamoja na wanahabari waliokuwepo katika eneo hilo walionekana kulipuka kwa shangwe na kuwapokea wachimbaji hao ambao kati yao walikuwemo wenye uwezo wa kuongea ambao walisimulia tukio lilivyokuwa pamoja na kusema kuwa walikuwa wamajawa na hofu wakiamini kuwa wamesahaulika.
Awali kabla ya kuokolewa, yalifanyika mawasiliano ya kuwatumia ujumbe kwa kutumia bomba ili waseme wako wangapi na majina yao, ambapo walisema kuwa wako 15 na kwamba walikuwa na njaa na walihitaji maji, soda, uji n.k
Hizi ni baadhi ya picha na video fupi zinazoonesha zoezi la uokoaji lilivyokuwa ambapo watu hao akiwemo raia wa China wamepatiwa huduma ya kwanza na kisha kupelekwa hospitali kwa uchunguzi zaidi.