Jumanne , 6th Dec , 2016

Mkurugenzi wa ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Salum Madadi amesema mchezaji wa mpira wa miguu kuwa katika mahusiano ya kimapenzi au kufanya starehe wakati wa mapumziko ya ligi, hakuathiri kiwango chake chake uchezaji kama inavyodaiwa.

Salum Madadi (Kulia) akiwa katika kipindi cha 5Sports. Wengine ni watangazaji wa kipindi hicho

 

Madadi ambaye ni mkufunzi wa makocha ambaye pia amewahi kuifundisha timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars, ametoa neno hilo akiwa katika kipindi cha 5Sports cha EATV kinachoruka kila Jumatatu saa 3:30 Usiku.

Madadi amesema hakuna ukweli juu ya dhana hiyo, na kwamba mchezaji yoyote bila kujali kama ameoa au ana mahusiano anaweza kuwa mchezaji mzuri kwakuwa mambo hayo hayategemeani.

Kuhusu wachezaji kujihusisha na starehe katika kipindi cha mapumziko ya ligi, Madadi alisema "starehe haziwezi kushusha kiwango cha mchezaji, cha msingi mchezaji ajitambue, ajue nini cha kula, nini cha kuacha nini cha kufanya wakati gani"

Cristiano Ronaldo nje ya soka, katika kipindi cha mapumziko

Madadi alikuwa akizungumzia maandalizi anayopaswa kuwa nayo mchezaji katika kipindi ambacho ligi imesimama au iko mapumzikoni ili kulinda kiwango chake, ambapo alishauri wachezaji kuwa na utamaduni wa kushiriki katika michezo mingine tofauti badala ya kuacha kabisa mazoezi, lakini pia aliwataka kutoendelea kujihusisha na mchezo wa soka kwa nguvu ili kutengeneza hamu ya kucheza wakati ligi itakaporejea.

Kuhusu utamaduni wa kuwaweka kambini wachezaji, Madadi alisema haoni umuhimu wa kuwaweka kambini wachezaji, maana wachezaji wa kitanzania wanaweza kuwekwa kambini na kudhibitiwa lakini wakipata upenyo wanafanya mambo yasiyotakiwa kwenye michezo.

"Hapa kwetu lazima mchezaji awe kambini tofauti na wanavyofanya wenzetu..kikubwa ni kujitambua, nashauri tupunguze muda wa kuwaweka kambini maana hata hivyo" Amesema  .

Pia Madadi hakusita kuzishauri mamlaka husika kukazana na soka la vijana ili kuinua kiwango cha soka nchini.