Meneja Masoko wa East Africa Television Bw. Roy Mbowe, amesema mchakato huo utakuwa wenye kutenda haki kwa wasanii, tofauti na ambavyo baadhi ya watu hufikiria kuwa utakuwa wa upendeleo.
"Tumeona kuna maswali mengi kuhusu hili, labda nifafanue, mchakato wa kujipendekeza utakuwa hauna lawama, kwanza msanii atapendekeza kazi zake au meneja wake anaweza akapendekeza pia, baada ya hapo team ya 'academy' itachagua kazi za wasanii kumi kwenye kila kipengele, kazi ambazo zimekidhi vigezo vyote vinavyotakiwa, kwa kupigia kura, baada ya hapo zile kumi zitapitiwa na majaji, na wenyewe watapitisha kazi za wasanii watano tu kwenye kila kipengele hivyo hivyo kwa kuzipigia kura, na hizo ndizo zitakazopelekwa kwa wananchi kuzipigia kura, na mshindi kupatikana", alisema Roy Mbowe.
Bw. Mbowe amesema kwa kufanya hivyo kutaepuka malalamiko mengi ambayo wasanii huyatoa mara kwa mara, ikiwemo zile za msanii kutotaka kushiriki au kum-nominate bila mwenyewe kushiriki kwenye tuzo.
Mchakato wa kuchukua fomu za kujipendekeza, umeanza tar 13 Sep 2016 na utaisha tar 12 Oktoba 2016, saa 11 jioni, na fomu zote zitatakiwa zipelekwe kwenye ofisi za EATV Ltd zilizopo Mikocheni, jijini Dar es salaam.