
Waziri Mkuu akikagua Ofisi zake mpya mjini Dodoma.
Katika ziara hiyo aliyoifanya leo ambapo amesema ameridhishwa na namna kazi ya ujenzi inavyofanyika na kueleza kuwa Kazi ya ujenzi inaendelea vizuri na kuwa katika kipindi kifupi watakuwa wamekamilisha.
Amesema kutokamilika kwa ujenzi huo hauwezi kukwamisha adhma yake ya kuhamia Dodoma kwa sababu tayari inafahamika kuwa Makao Makuu ya Ofisi ya Waziri Mkuu yako Dodoma.
Amesema uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma hautokani na shinikizo la kisiasa bali ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao chimbuko lake ni agizo lililotolewa Oktoba Mosi, 1973 kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa chama cha TANU
“Tangu wakati huo Serikali zote ziliendelea kufanya juhudi mbalimbali za kuandaa miundombinu na hata awamu ya nne ilisimamia kwa kiwango kikubwa uwekaji wa miundombinu hiyo,” amesema.
“Pia tukumbuke kauli ya Mheshimiwa Rais aliyotoa kwenye hotuba yake ya Julai 23, 2016 alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM, na akairudia tena Julai 25, kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya Mashujaa na mimi siku hiyo hiyo nikaweka msisitizo,” amesema.
Amesema uamuzi wa Serikali ya awamu ya tano wa kuhamia Dodoma unakuja baada ya kuridhishwa na ujenzi wa miundombinu na maeneo ya kutolea huduma za kijamii kwa wageni na wenyeji ikiwemo Hospitali ya Benjamini Mkapa iliyopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) yenye uwezo wa kutibu magonjwa makubwa kama ya moyo na figo.
Waziri Mkuu amesema tayari Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) ina mpango kamambe (master plan) na ina viwanja vya kutosha kujenga makazi na ofisi mbalimbali.