Jumatatu , 13th Jun , 2016

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ametoa mwezi mmoja kwa Katibu Mkuu wa Wizara anayeshughulikia Sekta ya Mawasiliano na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu nchini (TTCL), kuhakikisha kituo cha kutunzia taarifa kinaanza kazi.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ametoa mwezi mmoja kwa Katibu Mkuu wa Wizara anayeshughulikia Sekta ya Mawasiliano na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu nchini (TTCL), kuhakikisha kituo cha kutunzia taarifa (Data Centre) kilichopo Kijitonyama Jijini Dar es Salaam kinaanza kufanyakazi.

Prof. Mbarawa ametoa agizo hilo kufuatia kukamilika kwa kituo hicho miezi kadhaa iliyopita na mahitaji ya wadau wa huduma ya kutunza kumbukumbu za taasisi zao katika kituo hicho kuongezeka.

Aidha, amezitaka asasi za seriakli na binafsi kutumia kituo hicho cha kisasa kuhifadhia taarifa zao ili kuzihakikishia usalama na uhakika wa kutumiwa wakati wowote.

Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua uwanja wa ndege wa Singida na mahali utakapojengwa uwanja mpya huku akisisitiza umuhimu wa mamlaka ya viwanja vya ndege nchini kusimamia kikamilifu ujenzi wa uwanja huo mpya ambao upembuzi yakinifu umeshahakamilika.

Aidha, ametaja viwanja vya ndege vinavyofanyiwa upembuzi yakinifu tayari kwa kuanza ujenzi kuwa ni pamoja na Lake Manyara, Musoma, Iringa, Tanga, Songea,Kilwa Masoko, lindi,Moshi,Njombe,Simiyu na Singida.