Jumanne , 5th Apr , 2016

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Iringa, imewafikisha mahakamani watumishi wanne wa serikali Mkoani Iringa wakiwemo wafamasia wawili wa Wilaya ya Iringa Mjini na Mufindi.

Mkuu wa TAKUKURU, mkoani wa Iringa,Eunice Mmari

Akizungumza na Waandishi wa Habari Mkoani humo Mkuu wa TAKUKURU, Eunice Mmari, amesema kuwa watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa na ubadhirifu wa fedha za Umma.

Bi. Eunice aliwataja wafamasia hao waliofikishwa Mahakamani kwa kuisababisha hasara Serikali ya shilingi milioni moja ni pamoja na Lucas Daniel, Mfamasia wa hospitali ya Mkoa wa Iringa, na Seleman Hamza, mfamasia wa hospitali ya Mufindi ambao wote wanashtakiwa kwa makosa ya wizi ya mali ya Umma.

Mbali na hao Afisa huyo Takukuru amesema kuwa wamewafikisha kortini Mwenyekiti na Afisa mtendaji wa kijiji cha Ilula Mwaya wilayani Kilolo kwa tuhuma za upotevu wa shilingi milioni 1 fedha za mapato ya kijiji hicho.

Aidha Bi. Eunice, ameeleza kuwa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita amesema TAKUKURU imeweza kufikisha kesi 17 mahakamani kati yake tano zimekwishatolewa hukumu.

Ameongeza kuwa Sekta ya Afya na Serikali za mitaa ndio zinazoongoza kwa kupokelewa kwa malalamiko mengi kutoka kwa Wananchi huku akiwataka wananchi wa Mkoa huo kutoa ushirikiano katika kupambana na rushwa.

Sauti ya Mkuu wa TAKUKURU, mkoani Iringa, Eunice Mmari, akiongelewa watu waliofikishwa Mahakamani