Nahodha msaidizi wa timu ya Tanzania ya watoto wa mitaani Frank Wiliam akimkabidhi kombe Waziri Mkuu Mizengo Pinda timu hiyo ilipotembelea Bungeni leo (April 11 2014)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameipongeza Timu ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania kwa kutwaa Kombe la Dunia huko Rio de Janeiro – Brazil.
“Mmetuwakilisha vyema, ninawapongeza sana, pia mmewapa moyo watoto wengine wote wenye vipaji maalum lakini hawakubahatika kuwa na makazi rasmi, hongereni sana” Rais amesema.
Timu hiyo ya watoto wenye umri chini ya miaka 16 (under 16) ilipangwa kundi la 2 ambapo wamekuwemo na Nchi za Argentina, Nicaragua,Philippines na Burundi na kulikuwa na makundi matatu.
Tanzania iliingia nusu fainali kwa kuwa mshindi wa pili na pia kuminyana na Marekani na kuichapa mabao 6-1 na baadae kuitoa Burundi kwa mabao 3-1.
“Hongereni kwa kujituma na kucheza kwa ustadi”. Rais amesema na kuwaasa watoto “ongezeni bidii, nidhamu na mazoezi ya kutosha na hakika mtafanikiwa zaidi na kulibeba jina la Tanzania mbali zaidi ya hapa katika ulimwengu wa soka duniani, kwani hakuna kisichowezekana kama mtazingatia maelekezo, mafunzo, bidii na nidhamu ya yote mnayofanya” Ameongeza .
*****Mwisho*****
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu – Dar es Salaam.
11 Aprili,2014