Jumatatu , 7th Sep , 2015

Mabingwa wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara Yanga SC wanatarajiwa kuingia kambini hapo kesho kwa ajili maandalizi ya mchezo wa ligi kuu inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi mwishoni mwa wiki.

Yanga SC wataanza na Coastal Union ya Tanga Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati mechi nyingine zote za ufunguzi zitachezwa Jumamosi viwanja mbalimbali hapa nchini.

Katibu mkuu wa Yanga SC, Dk Jonas Tiboroha timu itafanya mazoezi Dar es Salaam kabla ya kwenda Bagamoyo mara baada ya wachezaji waliokuwa kwenye majukumu ya kimataifa kurejea wote ndipo timu itakwenda Bagamoyo.

Yanga SC ilianza vizuri msimu baada ya kutwaa Ngao ya Jamii kwa ushindi wa penalti 8-7 dhidi ya Azam FC kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 na sasa inaingia kwenye mbio za kutetea taji.

Kabla ya Yanga SC na Coastal Jumapili, mechi za ufunguzi za ligi kuu Jumapili zitakuwa kati ya Ndanda FC na Mgambo Shooting, African Sports na Simba SC, Majimaji FC na JKT Ruvu, Azam FC na Tanzania Prisons, Stand United na Mtibwa Sugar, Toto Africans na Mwadui na Mbeya City na Kagera Sugar.