Jumamosi , 11th Jul , 2015

Wingu zito limetanda ndani ya CCM baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati kuu ya CCM kutokana na baadhi ya makada wa chama hicho kutofautiana na maamuzi yaliyofikiwa na kikao hicho kuhusiana na uteuzi wa majina matano ya wanachama wanaowania Urais.

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, akiongoza kikao cha Kamati Kuu ya CCM (CC) jana katika ukumbi wa White House mjini Dodoma.

Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM imemaliza zoezi la kuchagua wagombea watano wanaostahili kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho usiku wa kuamkia leo, huku kukiwa na dalili za kuwepo kwa mpasuko mkubwa ndani ya chama hicho.

Mpasuko huo unatokana na baadhi ya wajumbe wa kamati Kuu, ambao ni Dkt Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na alhaj Adam Kimbisa, kutamka hadharani kuwa hawakubaliani na wanajitenga na maamuzi ya kamati kuu, kwa kile walichokitaja kuwa ni kukiukwa kwa katiba na kanuni za chama.

Dkt Nchimbi ndiye aliyetoa tamko hilo kwa niaba ya wenzake ambapo ametaja kanuni zilizokiukwa kuwa ni pamoja na kamati ya maadili kujipa majukumu ya kupunguza majina ya wagombea ambapo majina yaliyopelekwa kamati Kuu yalikuwa ni pungufu ya waliogombea.

Aidha, Nchimbi ametaja ukiukwaji mwingine kuwa ni wa kipengele kinachoitaka kamati kuu kupitisha jina la mgombea mwenye mvuto na anayependwa na watu ndani na nje ya chama, lakini kinyume chake majina yenye mvuto yameachwa na kupitishwa watu aliodai kuwa ni dhaifu.

Awali, Katibu a Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, aliwaambia waandishi wa habari kuwa Kamati Kuu imekamilisha zoezi la kuwapata wagombea watano, ambao hata hivyo hakuwa tayari kuwataja kwa maelezo kuwa majina yatafahamika hii leo na baadaye saa nne asubuhi yatafikishwa kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu kwa ajili ya kuyajadili

Majina yaliyopitishwa na kamati kuu ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, Balozi Amina Ally, Waziri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa katiba na sheria, Asha Rose Migiro taarifa zaidi zitapatikana kesho asubuhi.

EMMANUEL NCHIMBI
Nape Nnauye akizungumzia Maazimio ya kamati Kuu