Jumanne , 24th Nov , 2015

Timu ya Taifa ya Zanzibar Zanzibar Heroes imetupwa nje ya michuano ya Kombe la CECAFA Chalenji katika hatua ya makundi baada ya kutandikwa bao 4-0 na timu ya taifa ya Uganda The Cranes katika michuano hiyo inayoendelea nchini Ethiopia.

Katika mechi ya leo, Zanzibar walionekana hawana nguvu ya mipango na muda mwingi The Cranes walitawala mchezo ambapo katiika dakika ya 10 Farouk Miya aliweza kuipatia timu yake The Cranes bao la kwanza ambalo lilidumu kwa dakika nne.

Dakika ya 14 Miya aliweza kuongeza bao la pili kwa njia ya penati iliyosababishwa na mlinda mlango wa Zanzibar Heroes Mwadini Ally ambapo alipewa kadi nyekundu iliyomtoa nje mshambuliaji Amme Ally huku bao likidumu mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika.

Kipindi cha pili kilianza huku Uganda wakionekana kutafuta bao lingine na ndani ya dakika ya 48 The Cranes iliweza kupata bao la tatu kupitia kwa mshambuliaji wake Erisa Ssekisambu

Dakika ya 73 Zanzibar Heroes walipata pigo baada ya Mudathir Yahya kupata kadi nyekundu iliyotokana na kucheza rafu na dakika ya 78 Denis Okoth aliweza kuikamilishia The Cranes bao 4-0.