
Baadhi ya wachezaji wa Yanga
Ushindi huo unaifanya Yanga kuwa timu ya kwanza kwa siku ya leo kufunzu raundi ya 6 ambayo ni ya 16 bora na sasa inasubiri droo itakayofanywa baadaye ili kujua itakutana na nani katika hatua hiyo.
Katika mchezo wa leo, kikosi cha Yanga kilikuwa na utofauti mkubwa ambapo katika eneo la ulinzi wa katikati, alichezeshwa Oscar Joshua na Andrew Vincent 'Dante', wakati Haruna Niyonzima akipumzishwa na eneo la kati kuachiwa Mzimbabwe, Thaban Kamusoko, huku safu ya ushambuliaji akiachiwa Amis Tambwe na Saimon Msuva na langoni akisimama Benno Kakolanya.
Mabao ya Yanga ambayo imeutawala zaidi mchezo huo yamefungwa na Amis Tambwe dakika ya 20 akimalizia vizuri pande la Msuva, Kamusoko dakika ya 37 kwa shuti la mbali, Saimon Msuva dakika ya 53 kwa mkwaju wa penati baada ya kuangushwa katika eneo la hatari, na kinda Yusuph Mhilu ambaye amekamilisha karamu hiyo kwa kumalizia kwa kichwa kros ya Matheo Anthony iliyopanguliwa na kipa wa Ashanti dakika ya 89.
Bao la kufutia machozi la Ashanti lilipatikana dakika ya 62 kutokana na makosa ya Dante aliyeteleza na mpira kupokwa na straika wa Ashanti aliyembua kiufundi kipa wa Yanga.
Mchezo mwingine uliopigwa leo umeshuhudia Mbao Fc ikiichapa Alliance, zote za Mwanza mabao 2-1 na hivyo kufanikiwa kusonga mbele pamoja na Yanga huku mechi ya Majimaji na Mighty Elephant ikiahirishwa.