
Mchezo wa Yanga na Ndanda Fc
Ndanda Fc ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 16 ya mchezo kupitia kwa Nassor Hashim kabla ya Yanga kurudi mchezoni na kusawazisha katika dakika ya 23 kupitia kwa mchezaji Jaffary Mohamed ambaye alianza kwa mara ya kwanza katika kikosi hicho msimu huu.
Kwa matokeo hayo sasa Yanga inasalia katika nafasi yake ya tatu ikiwa na alama 26 baada ya kushuka dimbani michezo 10, alama ambazo zinaifanya kuwa sawa na Simba yenye alama hizo katika nafasi ya pili, ikiizidi kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa.
Yanga imeshindwa kuondoka na alama zote tatu kwa mara ya kwanza tangu Septemba 30 katika mchezo dhidi ya mahasimu wao Simba, mchezo ambao ulimalizika kwa suluhu ya bila kufungana.
Matokeo ya michezo mingine ni katika mchezo wa mapema zaidi uliozikutanisha Kagera Sugar dhidi ya Azam Fc, ambapo Azam Fc imeibuka na ushindi wa bao 1-0, bao pekee lililofungwa na mshambuliaji Donald Ngoma ambaye alipewa kadi nyekundu katika kipindi cha pili cha mchezo.
Mchezo uliochezwa saa 10:00 jioni, umeshuhudia Mwadui Fc ikitoka sare ya bila kufungana na Tanzania Prisons katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.