Ijumaa , 12th Feb , 2016

Mabingwa watetezi wa Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara Yanga SC wameondoka hii leo wakiwa na kikosi kizima kwenda mjini Curepipe, Mauritius kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Cercle de Joachim.

Kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm ameamua kubeba kikosi chake chote, kwa kuwa baada ya mchezo huo Jumamosi, ndege waliyokodi kwa ajili ya safari hiyo itaichukua timu hiyo kuipeleka Pemba, visiwani Zanzibar kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya mchezo wake wa Ligi kuu dhidi ya watani wao wa jadi Simba SC utakaopigwa Februari 20 Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Awali, Yanga SC ilipanga kuondoka nchini Jumatano ya Februari 10 kwa ndege ya Afrika Kusini (SA), ambalo lilishindwa kuwapatia ndege ya kuunganisha mapema mjini Johannesburg, kwenda Curepipe.

Kwa sababu hiyo, Yanga SC ikaachana na SA na kuamua kukodi ndege ya ATC ili kuepuka kuwachosha wachezaji wake kwa safari ndefu.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Jumamosi kuanzia Saa 9:30 Alasiri kwa saa za Mauritius Uwanja wa Curepipe mjini Curepipe kabla ya timu hizo kurudiana wiki mbili baadaye Dar es Salaam.

Kikosi kilichoondoka leo hii ni
Makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’ na Benedicto Tinocco.
Mabeki; Juma Abdul, Mbuyu Twite (DRC), Oscar Joshua, Mwinyi Hajji Mngwali, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Vincent Bossou (Togo) na Pato Ngonyani.
Viungo ni; Said Juma ‘Makapu’, Salum Telela, Thabani Kamusoko (Zimbabwe), Haruna Niyonzima (Rwanda), Simon Msuva, Issoufou Boubacar (Niger), Godfrey Mwashiuya na Deus Kaseke.
Washambuliaji ni; Malimi Busungu, Paul Nonga, Amissi Tambwe (Burundi) na Donald Ngoma (Zimbabwe).