Jumamosi , 16th Jul , 2016

Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga SC leo watakuwa katika kibarua cha kusaka ushindi wa kwanza katika Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika, watakapomenyana na Medeama ya Ghana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kikosi cha Yanga

Katika mchezo wa leo, Yanga itawakosa wachezaji wake watatu tegemeo, beki wa kushoto Mwinyi Hajji Mngwali, viungo Deus Kaseke na Geoffrey Mwashiuya ambao wote ni majeruhi.

Aidha, Yanga itaendelea kumkosa beki wake mpya wa kulia, Hassan Kessy ambaye klabu yake ya zamani, Simba SC imegoma kumuidhinisha achezee klabu mpya.

Mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe alikuwa anasumbuliwa na Malaria kwa wiki yote hii, lakini tangu juzi amefanya mazoezi kikamilifu na wenzake, kuashiria kwamba anaweza kucheza leo.

Medeama iliyowasili Alhamisi Dar es Salaam nayo haijashinda mechi baada ya kufungwa ugenini na TP Mazembe 3-1 na kulazimishwa sare ya 0-0 nyumbani na MO Bejaia.

Huo utakuwa mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza na wa tatu kwa washindi hao wa mataji yote Tanzania Bara, baada ya awali kufungwa mechi mbili, moja ugenini na moja nyumbani.

Yanga ilianza kwa kuchapwa 1-0 na Mouloudia Olympique Bejaia nchini Algeria kabla ya kufungwa 1-0 tena na TP Mazembe ya DRC mjini Dar es Salaam.

Na leo timu ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm inacheza mechi ya pili mfululizo nyumbani ikisaka ushindi wa kwanza, ili kurejesha matumaini ya kwenda Nusu Fainali.

Mchezo mwingine wa kundi hilo utachezwa kesho, Mouloudia Bejaia wakiikaribisha TP Mazembe Uwanja wa Unite Maghrebine mjini Bejaia.

Mechi za Kundi B Kawkab Marrakech watakuwa wenyeji wa ndugu zao, FUS Rabat Uwanja wa Grand Marrakech, wakati Etoile Sahel wanaikaribisha Al Ahly Tripoli ya Libya leo Uwanja wa Olympique de Sousse, Tunisia.