Yanga itacheza mchezo wake wa Raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Cercle de Joachim siku ya Jumamosi ya Febuari 13 mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es salaam mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro amesema timu itaondoka ikiwa na kikosi kile kile kilichopangwa awali cha wachezaji 21 pamoja na viongozi na mkuu wa msafara kwa ndege ya kukodi.
Muro amesema, kuahirishwa kwa safari imetokana na ratiba ya ndege waliyotakiwa kuondoka nayo ambayo ingewafanya wachezaji kuchoka zaidi hivyo kukodi ndege kutasaidia wachezaji hao kufika na kufanya maandalizi kwa ajili ya mechi hiyo ya klabu bingwa Afrika pamoja na maandalizi ya mechi ya ligi kuu dhidi ya watani zao Simba SC.
Muro amesema, mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo dhidi ya Cercle de Joachim ambao utachezwa usiku kikosi kitaondoka kutumia ndege hiyohiyo ya kukodi kuelekea visiwani Pemba kuweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba SC utakaopigwa Februari 20 uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Muro amesema, lengo la kuiondoa timu usiku kuelekea Pemba ni kuhakikisha wanawapa muda wachezaji na kutoa fursa kwa timu kupata wakati mzuri na kupunguza uchovu ili kupata wakati mzuri wa kujiandaa dhidi ya watani wao wekundu wa Msimbazi Simba SC.





.jpg?itok=5cvL0YaP)