Ijumaa , 10th Sep , 2021

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa leo Bungeni, amewapongeza Wawekezaji na Watendaji wa vilabu vya Simba SC,Yanga SC pamoja na Azam FC kkwa uwekezaji mkubwa na usimamizi mzuri wa vilabu hivyo kwenye soka letu ambalo limeanza kuzaa matunda.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa akiongea akiwa bungeni leo jijini Dodoma.

Sambamba na pongezi hizo Mh. Majaliwa ameupongeza uongozi wa Shirikisho la soka nchini (TFF) chini ya Rais wake, Wallace Karia kwa usimamizi mzuri wa soka nchini.

Pia Waziri mkuu amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha na kuvutiwa wawekezaji katika tasnia ya michezo lengo ni kukuza vipaji na kuibua vipaji mbali mbali ilikuweza kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi na hivyo kuimarisha ajira, mapato yatokanayo na mchezo pamoja na mchango katika sekta hiyo.

Kwa upande mwingine, waziri Majaliwa ameipongeza timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars kufuatia ushindi dhidi ya Madagascar siku ya Jumanne na hivyo kuongoza kundi J kwenye mzunguko wa pili kuwania kufuzu michuano ya kombe inayotajari kufanyika nchini Qatar 2022.

Kuelekea mashindano ya COSAFA kwa upande wa wanawake yanayotarajia kuanza tarehe 28 Septemba mwaka huu, Mh. Majaliwa amewatakia kila la kheri Twiga stars kwenye michuano hiyo itakayofanyika nchini Afrika Kusini.