Jumatano , 20th Mei , 2015

Wanariadha wawili kati ya watatu waliosaini mkataba wa kujiunga na Kipkeino kilichopo Eldoret nchini Kenya kwa ajili ya kujiandaa na michezo ya Olimpiki Rio 2016 wameshindwa kuondoka nchini baada ya kuchelewa kupata ruhusa kutoka kwa mwajiri wao.

Akizungumza na East Africa Radio, Katibu wa Chama cha Riadha nchini RT, Suleiman Nyambui amesema, Fabian Joseph na Bazil John wameshindwa kuondoka nchini Jumamosi iliyopita kwenda Kenya kujiunga na kituo hicho hadi watakapopata kibali kutoka kwa mwajiri wao.

Nyambui amesema, mwanariadha Fabian Sulle ndiye mwanariadha pekee kutoka hapa nchini aliyejiunga na kituo hicho baada ya kuondoka nchini Jumamosi akiwaacha wanariadha wenzake wakiendelea kujifua wakisubiri hatma yao.

Nyambui amesema, kambi hii ni ya muda mrefu kwa kuwa itadumu hadi Septemba 2016 hivyo wanasubiri kibali cha kuondoka nchini na wanatarajiwa kuondoka siku yoyote kuanzia leo.