
Kikosi cha Njombe Mji kilichocheza ligi kuu msimu wa 2017/18.
Akiongea na www.eatv.tv msemaji wa timu hiyo Hassan Macho, amesema kamati imefikia uamzi huo ili kuweza kuirudisha kwa wananchi wa Njombe ambao kimsingi ndio wamiliki wa timu baada ya wao kujitahidi kuiendesha kwa kujitolea lakini uwezo wao umefika mwisho.
''Ni kweli kamati imekaa na kufikia uamzi huo, tunaikabidhi timu kwa chama cha soka cha mkoa (NJOREFA), ili wao wafanye taratibu za kuwakabidhi wamiliki ambao ni wananchi ili waweze kuisaidia timu yao ishiriki ligi daraja la kwanza msimu ujao'', amesema.
Macho ameongeza kuwa tangu uongozi uliopo umalize muda wake, wamekuwa wakiitisha uchaguzi bila mwitikio wa wananchi hivyo wameona ni busara kukabidhi timu kuliko kuendelea kuwa madarakani kinyume cha sheria.
Hivi karibuni aliyekuwa mwenyekiti wa timu hiyo Erasto Mpete, alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo kwa kile alichoeleza ni kubanwa na majukumu. Njombe Mji imeshuka daraja msimu huu baada ya kumaliza katika nafasi ya mwisho ikicheza mechi 30, kushinda 4 na sare 10 huku ikifungwa mechi 16.