Jumatano , 7th Sep , 2016

Viongozi wa vilabu vya Soka nchini wametakiwa kujitokeza kuangalia vipaji vya vijana wanaoshiriki mashindano ya Airtel Rising Stars Kitaifa ili kuweza kupata vipaji vipya vitakavyoendeleza soka hapa nchini.

Moja kati ya mechi za vijana katika michuano ya ARS inayoendelea Dar es Salaam

Balozi wa michuano ya Airtel Rising Stars Zamoyoni Mogela amesema, viongozi wa vilabu wanatakiwa kutumia fursa iliyopo ya kuangalia na kuchukua vijana wenye vipaji kuviendeleza ili kuweza kuwa na wachezaji wapya na wazuri ambao watakuwa na msaada kwa Taifa hapo baadaye.

Mogela amesema, vijana wengi ambao wanashiriki michuano hiyo wanaonyesha viwango vya hali ya juu hivyo kama viongozi hawatajitokeza vitapotea na hata nchi itakosa vipaji vipya ambavyo vitakuwa na faida katika soka la Tanzania.

Kwa upande wake Afisa Uhusiano Airtel Tanzania Jane Matinde amesema, ushindani umekuwa ni mkubwa katika mashindano hayo hususani kwa timu kutoka mikoani ambazo hapo awali zilikuwa hazifanyi vizuri katika ngazi ya mkoa.

Michuano hiyo imeanza kutimua vumbi hapo jana katika hatua ya ngazi ya taifa na inatarajiwa kufikia tamati siku ya Jumapili kwa kuchezwa mchezo wa fainali.