'Vibonde' wa Yanga watua Dar kwa kishindo

Thursday , 16th Feb , 2017

Wapinzani wa Yanga katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika timu ya Ngaya kutoka Comoro wamewasili leo jijini Dar es Salaam tayari kabisa kwa mchezo wa marudiano utakaochezeshwa na waamuzi kutoka nchini Uganda.

Kikosi cha Ngaya kutoka Comoro kikiwasili hii leo Uwanja wa Ndege Jijini Dar es salaam

 Timu hiyo imewasili leo saa saba na nusu mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), huku ikiwa imeongozana na baadhi ya viongozi wake.

Mara baada ya kuwasili timu hiyo ilipokelewa na wananchi wa nchi hiyo wanaoishi hapa nchini hata hivyo viongozi wa timu hiyo hawakuwa tayari kuzungumza chochote na wanahabari badala yake walipiga picha ya pamoja na wachezaji na kisha kupanda kwenye magari na kuondoka. 

Kuelekea katika mchezo huo utakaopigwa Jumamosi hii katika dimba la Taifa, Kocha Msaidizi wa Yanga Juma Mwambusi amesema, bado wanaangalia umuhimu wa dakika 90 za marudiano ili kuhakikisha wanapata ushindi wa nyumbani.

Akizungumza jijini Dar es salaam Kocha Mwambusi amesema, wanaamini kiwango cha wapinzani wao ni kizuri na bado watahitaji kupambana lakini kwa upande wao wamejipanga ili kuhakikisha wanapata ushindi utakaowapa nafasi ya kusonga mbele.

“Tunatambua umuhimu wa mchezo wetu wa marejeano ambao utafanyika siku ya Jumamosi, Ngaya siyo timu mbaya kwasababu hata ukiangalia dakika tuliyoanza kupata goli la kwanza inaonesha ni kiasi gani wamejipanga, kikubwa tunawaomba mashabiki wetu na wanamichezo wajitokeza kwa wingi kuipa sapoti timu yao,” alisema.

Katika mchezo wa Kwanza Yanga ilishinda mabao 5-1, hali inayoashiria ugumu kwa timu hiyo ya Comoro kuvuka katika hatua hiyo.