Alhamisi , 28th Mei , 2015

Timu za majiji kutoka Tanzania zimejipa matumaini ya kuingia katika hatua ya fainali na hatimaye kuibuka na ushindi katika mashindano ya mpira wa kikapu Afrika mashariki na kati yanayoendelea uwanja wa ndani wa Taifa jijini Dar es salaam.

Akizungumza na East Africa Radio, mmoja wa wana kamati ya maandalizi ya michuano hiyo hapa nchini, Robert Manyerere amesema, kwa upande wa timu za wanawake zipo timu tatu za Nairobi, Kampala na Dar es salaam na mchezo wa mwanzo hapo jana Dar es saalaam ilipoteza mchezo hivyo anaamini katika mchezo wa marudiano itafanya vizuri na kuweza kufika nafasi za juu.

Manyerere amesema, kwa timu za wanaume Dar stars iliyoanza vizuri kwa kuishinda Mogadishu ina nafasi nzuri ya kufika mbali huku kwa upande wa Dar City ikipoteza mchezo wake hapo jana lakini anaamini itafanya vizuri ili kuweza kuipa Tanzania sifa katika mashindano hayo.