Alhamisi , 5th Nov , 2015

Timu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars imepangwa kuanza na Zimbabwe katika raundi ya kwanza ya mchujo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya wanawake nchini Cameroon mwaka 2016.

Kwa mujibu wa Ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), mechi za kwanza zitachezwa kati ya Machi 4, 5 au 6, wakati marudiano yatakuwa kati ya Machi 18, 19 au 20, mwakani.

Twiga ikifanikiwa kuitoa Zimbabwe, itamenyana na mshindi kati ya Zambia na Namibia, mechi za kwanza zikichezwa kati ya Aprili 8, 9 au 10 na marudiano April 22, 23 au 24.

Katika mechi zote Tanzania itaanzia nyumbani na baada ya hatua hizo, timu saba zitaungana na wenyeji, Cameroon kwa ajili ya fainali za mataifa ya Afrika kwa wanawake kuanzia Novemba 19 hadi Desemba 3 mwaka 2016.