Jumatatu , 31st Aug , 2015

Kocha mkuu wa timu ya Tanzania Taifa Stars Charles Mkwasa amesema vijana wake wapo tayari kuwavaa Nigeria Septemba 05, 2015 katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za AFCON mwaka 2017.

Mkwasa ambaye yupo nchini Uturuki na kikosi cha timu ya Taifa kambini kwa mazoezi ya takribani wiki moja, amesema anaona dalili nzuri ya vijana kuelekea katika mchezo huo dhidi ya Nigeria kwani vijana wameonesha mabadiliko makubwa katika mazoezi ambapo yamewajenga na wana uwezo wa kucheza kwa nguvu muda wote na wanakaba na kushambulia kwa pamoja.

Mkwasa amesema kambi hiyo imekuwa na faida kubwa kiufundi, kufuatia kupata nafasi ya kukaa sehemu tulivu na wachezaji kuwapa mazoezi ambayo waliyapanga katika program hiyo ya kambi nchini Uturuki.

Taifa Stars imemaliza mazoezi ya mwisho leo asubuhi kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani Tanzania kwa maandalizi ya mwisho ya mchezo huo.