Trent- Alexander Arnold amegomea mkataba mpya wa kusalia kikosi cha Liverpool na kuamsha presha kwa Mabosi wa klabu hiyo juu ya mustabali wa mchezaji huyo ndani ya timu hiyo. Taarifa zinazowastua zaidi Uongozi wa Majogoo wa Jiji ni kuhusiana na jina la nyota huyo kuwepo kwenye listi ya Wachezaji wanaohitajika kwenye kikosi cha Real Madrid ya Hispania dirisha kubwa usajli mwezi Julai 2025.
Mkataba wa Trent ndani ya Liverool unatamatika mwishoni mwa msimu wa 2024-2025.
Trent - Alexander Arnold amezua hofu ndani ya klabu yake baada ya kuonekana kushindikana katika majadiliano juu ya mkataba mpya na mchezaji huyo. Trent amekuwa mmoja wa Wachezaji wa muhimu kwenye kikosi cha Liverpool kwa muda mrefu tangu alipopandishwa kukitumikia kikosi cha kwanza cha Majogoo ya Jiji mwaka 2016 na aliyekua kocha wa timu hiyo Jurgen Klopp.
Trent raia wa Uingereza amejiunga na kituo cha kufundisha mpira cha Liverpool mwaka 2004, amedumu kwenye kikosi cha The Reds kwa miaka 20. Taarifa kutoka ndani ya klabu ya Liverpool zinasema mazunguzmzo juu ya mkataba na mchezaji huyo yamekuwa magumu na kuna hofu huenda akaondoka mwishoni mwa msimu huu wa 2024-2025 ambapo mkataba wake utatamatika.
Real Madrid ya Hispania imeweka jina la beki wa kulia wa timu ya taifa ya England kama mchezaji ambaye wanayehitaji kumsajili kwenye dirisha kubwa la usajili majira ya kiangazi Julai 2025. Mabingwa mara 15 wa kombe la klabu bingwa Ulaya wanamuona Trent Arnold kama mbadala sahihi wa beki wao raia wa Hispania aliye majeruhi kwa sasa Dani Carvajal.
Liverpool inayonolewa na Kocha raia wa Uholanzi Arne Slot imeanza vizuri msimu wa 2024-2025 ligi kuu Uingereza inashika nafasi ya kwanza katika msimamo ikiwa imejikusanyia alama 18 baada ya kucheza michezo saba ikifuatiwa na Mabingwa watetezi wa ligi hiyo Manchester City yenye alama 17 nafasi ya pili baada ya michezo saba.
Beki huyo wa kulia timu ya taifa ya England amekuwa mchezaji muhimu kwenye mafanikio ya Liverpool chini ya Klopp baada ya kuiwezesha timu hiyo yenye makazi yake kwenye dimba la Anfield kushinda kombe la ligi kuu Uingereza msimu wa 2019-2020 na ubingwa wa ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu wa 2018-2019 baada ya kuifunga Tottenham kwenye mchezo wa fainali.