
Wachezaji Harry Kane mwenye jezi nyekundu na Dele Alli mwenye jezi nyeupe.
Jumla ya wachezaji 9 kutoka klabu ya Tottenham ambayo ilimaliza katika nafasi ya 3 kwenye ligi kuu ya England msimu wa 2017/18, wanayatumikia mataifa yao. Nyota hao ni Danny Rose, Eric Dier, Harry Kane, Kieran Trippier, Dele Alli wote England, Jan Vertonghen, Toby Alderweireld, na Mousa Dembele wote Belgium na Hugo Lloris wa Ufaransa.
Timu ya pili kuwa na wachezaji wengi zaidi katika hatua ya nusu fainali ni mabingwa wa Ligi kuu ya England Manchester City wenye wachezaji 7 sawa na Manchester United ambayo nayo inawachezaji 7. Chelsea kutoka England nayo inawachezaji 6 katika timu 4 zilizofika nusu fainali.
Aidha vilabu vinne ambavyo ni Liverpool, PSG, Barcelona na Monaco vyote vina wachezaji wanne. Kwa idadi hiyo ya wachezaji kutoka England unaifanya ligi kuu ya EPL kuwa na wachezaji 40 katika nusu fainali. La Liga ina wachezaji 12 huku Ligue 1 ikiwa na wachezaji 11. Bundesliga ina wachezaji 9 na Serie A ikiwa nao 8.
Mechi za nusu fainali zitaanza kutimua vumbi kesho Jumanne Julai 10, ambapo Ufaransa watakipiga na Ubelgiji huku Jumatano Croatia watashuka dimbani kucheza na England. Mechi ya fainali itapigwa Julai 15 kwenye uwanja wa Luzhniki uliopo jijini Moscow.