The Tanzanite yarejea nchini kutokea Nigeria

Monday , 18th Sep , 2017

Mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu Kombe la dunia kwa wasichana chini ya umri wa miaka 20 kati ya The Tanzanite na Nigeria utapigwa Oktoba 1 kwenye uwanja wa Azam Complex.

The Tanzanite ilipoteza mchezo wa mkondo wa kwanza ugenini dhidi ya Nigeria mabao 3-0 siku ya Jumamosi na leo imerejea nchini ikitokea Nigeria tayari kwa kuanza maandalizi ya mchezo wa marejeano.

Katika mkutano na waandishi wa habari baada ya kuwasili kocha wa kikosi hicho Sebastian Nkoma amesema ameridhishwa na kiwango kilichooneshwa na vijana wake hivyo anaamini watapata matokeo mazuri kwenye mchezo wa Oktoba 1.

Mkuu wa msafara wa The Tanzanite Amina Karuma ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake Tanzania (TWFA) amesema anashukuru wachezaji wote ni wazima na wataendelea na kambi ili kujiandaa na mchezo wa marudiano huku akiahidi kuwatafutia mechi ya kirafiki kabla ya kuwakaribisha Nigeria.