Jumatatu , 15th Dec , 2014

Shirikisho la Soka nchini TFF, limesema Jamii inatakiwa kuwa na miundombinu ya kimichezo na kutokuwa na tamaduni juu ya watoto wa kike kutoishiriki michezo suala ambalo linachangia kuendelea kufanya vibaya katika michezo hapa nchini.

Akizungumza na Ea Radio jijini Dar es salaam wakati wa ufunguzi wa kozi ya makocha wa mpango wa Grassroots unaolenga kwa walimu 34 kutoka mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es salaam, Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Celestine amesema Programu hii ya mwaka 2013/2017 ilianza lakini haijafanikiwa kufikia malengo kutokana na maeneo mengi kutokuwa na viwanja kwa ajili ya kuendeshea kozi hii.

Celestine amesema jamii nyingi zina tamaduni kuwa mtoto wa kike haruhusiwi kushiriki michezo suala ambalo sio kweli hivyo jamii inatakiwa kuwaendeleza watoto wa kike na wa kiume ili kuweza kupata jamii ya michezo hususani mpira wa miguu hapa nchini na kuweza kupata timu bora ambayo itaitangaza nchi.

Celestine amesema mwishoni mwa mwaka huu wanatarajia kuwa na mashindano ya vijana chini ya miaka 13 yatakayofanyika mkoani mwanza hivyo michuano hiyo pia itatoa nafasi kwa vijana hao kujifahamu wao pamoja na vipaji vyao kwa ujumla.