Alhamisi , 4th Aug , 2022

Kocha wa Manchester United Erik Ten Hag amesema Cristiano Ronaldo anaweza kufaa katika aina yake ya uchezaji lakini atahitaji kujiimarisha kwanza kabla ya kupata nafasi ya kuthibitisha kuwa anastahili nafasi katika kikosi cha kwanza.

Kocha Erik Ten Hag akimwelekeza jambo Ronaldo katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Rayo Vallecano jumapili iliyopita.

Ronaldo hakuwepo katika kikosi cha United kwenye ziara ya maandalizi ya msimu mpya nchini Thailand na Australia, na pia alikosekana katika mchezo wa kirafiki waliofungwa goli 1 kwa 0 dhidi ya Atletico Madrid, lakini alicheza dakika 45 za kipindi cha kwanza katika mchezo dhidi ya Rayo Vallecano uliomalizika kwa sare ya goli 1 kwa 1 katika dimba la Old Trafford Jumapili iliyopita.

Ten Hag aliongeza kusema mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno anaweza kufaa katika mfumo wake wa jinsi anavyotaka United icheze ila kwanza inabidi ajiimarishe kimwili na aonyeshe kwamba anaweza kutimiza majukumu ipasavyo.

Mustakabali wa Ronaldo ndani ya United umekuwa wa hali ya sintofahamu baada ya vyombo vya habari vya Uingereza kuripoti kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 37 aliomba kuondoka klabuni hapo ili acheze ligi ya mabingwa barani Ulaya.

United ambayo itacheza ligi ya Europa msimu huu, wataanza kinyang’anyiro cha ligi kuu ya Uingereza siku ya Jumapili dhidi ya Brighton & Hove Albion.