Ijumaa , 12th Mei , 2017

Klabu ya Simba SC imefanikiwa kurudi kileleni rasmi baada ya kuichakaza timu ya Stand United bao 2-1 katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Wachezaji wa Simba pamoja na Stand United wakiwa uwanjani Leo Taifa

Wekundu wa Msimbazi wanafikisha pointi 65 baada ya ushindi wa leo wakiwa wamecheza mechi 29, mbili zaidi ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 62, ambao wanaweza kurudi kileleni kwa mabao zaidi, wakiifunga Mbeya City kesho Uwanja wa Taifa.
Katika mchezo huo uliojawa vita ya piga nikupige, Stand United ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata kulichungulia lango la wapinzani wao kwenye sekunde ya 58 tu ya kipindi cha kwanza kupitia mchezaji wake Selemani Kassim Selembe.

Simba walifanikiwa kusawazisha bao hilo katika dakika ya 23 kupitia kwa mshambuliaji wake, Juma Luizio anayecheza kwa mkopo kutoka Zesco United ya Zambia, aliyefunga kwa kichwa akiunganisha krosi ya winga Shiza Kichuya.

Kama hiyo haitoshi ilipofikia dakika 35 za mchezo Juma Luizio alipaitia timu yake bao la pili na kuisababishia timu yake kuwa mbele zaidi kwa bao dhidi ya wapinzani wao mpaka kipenga cha mwisho kilipo pulizwa kutoka kwa muamuzi wa mchezo wa leo.