Ijumaa , 30th Oct , 2015

Ligi kuu ya soka Tanzania Bara inaendelea hapo kesho katika mzunguko wake wa 10 kwa michezo minne kuchezwa ambapo Simba itaikaribisha Majimaji ya Songea uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Nahodha wa Simba SC Mussa Hassan Mgosi amesema, wanaamini watafanya vizuri na kocha ameshaangalia makosa yaliyoonekana katika mechi iliyopita dhidi ya Coastal Union hivyo hakuna kitakachowazuia kesho kushindwa kuibuka na pointi tatu.

Mgosi amesema, katika kikosi cha Simba hakuna anayetegemewa katika kufunga bali ni bahati na mara nyingi hudondokea kwa mganda Hamis Kiiza na kwa upande wao kama kikosi hawaangalii nani kafunga bali wanaangalia point tatu katika kila mchezo.

Mgosi amesema, ligi ni ngumu na timu zote zilizo juu au chini katika msimamo wa ligi zina upinzani katika kila mechi, hivyo kila timu inatakiwa kufanya kama walivyojiandaa kwa msimu huu na hata kwa upande wao hawawezi kuidharau timu yoyote kwani kila timu ina upinzani lakini kwa upande wao kila mechi ni fainali.

Mechi nyingine zitakazopigwa hapo kesho ni Yanga watakaokuwa ugenini dhidi ya Kagera Sugar uwanja wa Ally Hassani Mwinyi Mjini Tabora huku Mtibwa Sugar wakiwakaribisha Mwadui FC uwanja wa Manungu mjini Morogoro na Coastal Union ikiikaribisha Mbeya City uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Ligi hiyo itaendelea Jumapili ambapo Azam FC wataikaribisha Toto Africans uwanja wa Chamazi jijini Dar es salaam, African Sports wakiwa wenyeji wa JKT Ruvu uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga na wajelajela Tanzania Prisons wakiwakaribisha Ndanda FC uwanja wa Sokoine jijini Mbeya huku mzunguko wa kumi wa ligi hiyo ukihitimishwa siku ya Jumatatu kwa kuchezwa mchezo mmoja utakaowakutanisha Mgambo wakiwakaribisha Stand United uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.