Jumapili , 20th Oct , 2024

Mechi ya jana iliyochezwa kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es salaam ilikua mechi ya dabi ya nne mfululizo Simba SC inapoteza mbele ya Watani wao wa jadi Yanga SC. Haijawahi kutokea kwenye historia ya dabi ya Kariakoo timu moja kufungwa zaidi ya michezo miwili mfululizo.

Yanga SC imeshinda mchezo wa Dabi jana kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa kwa ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Wapinzani wao wa jadi timu ya Simba. Yanga ilicheza kwa heshima kubwa kwa kufahamu Simba SC ingekuja kwa nia ya kushambulia kuanzia dakika ya kwanza mchezo kutokana na matokeo ya nyuma dhidi ya Wapinzani wao. Ubora wa Yanga ni mkubwa sana na hii inajidhihirisha kutokana na kuchukua ubingwa mara tatu mfululizo huku ikiwa inatafuta ubingwa wake wa nne kama itafanikiwa kuutetea ubingwa wa ligi msimu huu wa 2024-2025. Ushidni wa jana ni wa nne mfululizo mbele ya Watani wao wa jadi na majirani zao mitaa ya Karikoo Simba SC, Simba imebadilika chini ya Kocha Fadlu Davies lakini bado haijawa timu kamili ambayo inayoweza kubishana na Yanga kutokana na uzoefu wa Yanga kucheza akitimu na utofauti wa madaraja ya mchezaji mmojammoja.

Yanga SC imeshinda mchezo wa Dabi uliokuwa unasubiriwa kwa hamu na Wadau wa soka nchini Tanzania, mchezo huu ulitengeneza shauku kubwa kwa Mashabiki wa timu za Simba na Yanga kutokana na matokeo ambayo Simba imekua ikiyapata mbele ya Wapinzani wao timu ya Yanga SC.

Mchezo wa jana umefikisha idadi ya michezo minne mfululizo timu ya Yanga imetoka na matokeo ya ushindi dhidi ya Simba SC, hii inatoa ishara ya kwamba kwa sasa ubora wa Wana Jangwani ni mkubwa ukilinganisha na  Wapinzani wao. Haijawahi kutokea kwenye michezo ya Dabi ya Kariakoo timu moja kufungwa kwenye michezo miwili mfululizo Yanga imeandika historia mpya ambayo inaweza kuchukua muda mrefu  kufikiwa na kuvunjwa.

Faida ambayo timu ya Wanachi inayo ni kikosi chake kimekaa pamoja kwa muda nrefu zaidi ya miaka mitatu huku maboresho yakiwa yanafanyika kwa kuingiza Wachezaji ambao wanaongeza ubora bila kuathiri mtiririko na mpangilio wa kiuchezaji ambao Mwalimu anautaka kutoka kwa Wachezaji wake.

Pili Yanga inanufaika na uwepo wa Wachezaji  wenye uzoefu na ukomavu mkubwa ambao wapo kwenye vilele vya uchezaji wao kwa pamoja, mfano Khalid Aucho, Mudathir Yahya, Aziz Ki, Pacome, Maxi Mpia, Kouassi Yao, Diara  na wengine wengi hivyo inawapa nafasi kubwa yakushinda michezo mikubwa na migumu kutoakana na uwepo wa kundi kubwa la Wachezaji wakomavu kwenye timu.

Tatu uwepo wa Miguel Gamondi kwenye benchi la ufundi la timu ya Yanga ubora wake kimbinu, kufahamu vizuri mpira wa Afrika pamoja na uwezo wa kuunganisha vipaji alivyonavyo kwenye timu, kujenga kikosi imara chenye ushindani wa namba kuanzia mazoezini mpaka kwenye mechi  na  kuifanya timu iendelee kuwa na njaa ileile ya mafanikio ni kazi kubwa  ambayo inafanywa na mkufunzi huyu raia wa Argentina.

Simba SC inawachezaji wengi vijana ambao wanacheza kwa kujituma na kupambana ila kila mchezaji  anacheza kivyake kutokana na bado timu haina muunganiko ambao unaiwezesha timu kucheza kitimu na kurahisiha maamuzii ya Wachezaji ndani ya uwanja. Wekundu wa Msimbazi bado wapo kwenye hatua ya kuijenga timu yao kama Watamaumini Mwalimu Fadlu Davies na kuwa na subira naye ninaimani atajenga kikosi imara kitakachosumbua kwa muda mrefu kwenye ligi ya Tanzania.