
Kikosi cha Serengeti Boys kikisherehekea kushika nafasi ya tatu kwenye mashindano ya mwaliko nchini India mwezi uliopita.
Nahodha wa Timu ya Taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 Serengeti Boys, Issa Abdi amesema mashindano ya vijana yaliyofanyika nchini India mwezi uliopita, yamewajenga vizuri, baada ya kukutana na mataifa yaliyondelea kisoka kama Marekani na Korea Kusini.
Abdi amesema wanataraji kambi ya Juni 13 mwaka huu kujiandaa kufuzu fainali za Africa mwakani dhidi ya Shelisheli baadae mwezi huu, itakuwa ya kufanyia kazi mapungufu waliyobaini nchini India.
Aidha kwa upande mwengine, Nahodha huyo anayecheza nafasi ya kiungo, aliyeibuliwa kwenye mashindano ya Copa Coca Cola mwaka juzi, amesema wameona tofauti ya watoto wa mataifa yaliyoendelea kisoka wanaandaliwa tangu chini, tofauti na wao kutoka nchi zinazoendelea, wanafanya jitihada zao binafsi kukuza vipaji vyao.