Jumatatu , 3rd Apr , 2017

Dakika 5 kati ya 10 za nyongeza zimetosha kuipa sare ya mabao 2-2 timu ya taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kama Serengeti Boys dhidi ya vijana wenzao kutoka Ghana, Black Starlets katika dimba la Taifa Dar es Salaam.

Mchezaji wa Serengeti Boys akichomoka katikati ya wachezaji wa Ghana

Katika mchezo huo wa Kimataifa wa kirafiki, Serengeti Boys  walielemewa katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo na kusababisha  wapinzani wao kujipatia bao la kwanza likifungwa na Sulley katika dakika 22 ya mchezo na hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Serengeti Boys walikuwa nyuma kwa bao hilo.

Baada ya kurudi kipindi cha pili Serengeti ilionesha jitihada zake za kuchungulia goli la wapinzani wake lakini juhudi hizo hazikuweza kuzaa matunda na matokeo yake waliweza kupachikwa bao la pili lilofungwa na Mensah katika dakika 74 ya mchezo kwa mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Mensah nje kidogo ya box na mpira huo kutinga moja kwa moja kimiani.

Kutokana na muda mwingi kupotea wakati wakati wa mchezo kulikosababishwa na wachezaji wengi wa Ghana kuanguka mara kwa mara, ilimlazimu mwamuzi kuongeza dakika 10 baada ya dakika 90 kumalizika ambapo katika dakika hizo 10 za nyongeza, Serengeti walionekana kupata uhai zaidi na nguvu ya kusawazisha mabao.

Kunako dakika ya 90 (+5) Serengeti Boys walipata penati iliyofungwa kiustadi wa hali ya juu na Makame na kufanikiwa kuandika bao la Kwanza.

Kama hiyo haitoshi, Serengeti waliongeza kasi ya mashambulizi na kufanikiwa kupata bao la pili katika dakika ya 90 (+11) likifungwa na Assad na kufanya matokeo yawe sare ya 2-2. 

Matokeo hayo ni heshima na faraja kwa watanzania kwa kwa kukataa kufungwa nyumbani mbele ya waziri anayehusika na michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe aliyekuwa mgeni rasmi kwa leo  

Serengeti imetumia mchezo huo kuwaaga watanzania kuelekea kwenye kambi maalumu nchini Morocco kujiandaa na fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 nchini Gabon.