Wachezaji wakiwa katika Mafunzo,mapema leo Chamazi
Siku ya pili ya mafunzo kwa wachezaji 72 wa kike na kiume kutoka mataifa 12 barani Afrika yanayofanyika katika uwanja wa Azam Complex imeendelea hii leo huku walimu kutoka shule ya mafunzo ya soka ya Manchester United wakifurahishwa na mwamko walionao vijana katika kujifunza soka.
Kocha mkuu kutoka shule ya kukuza vipaji ya Manchester United, Neil Scott, amesema wameanza vizuri mafunzo hayo yaliyofunguliwa rasmi jana, huku akisisitiza kuwa nidhamu na heshima kwa wachezaji ni misingi ya kufikia malengo yao ya kimichezo.
Washindi wa michuano ya mwaka jana ya Airtel Rising Stars iliyofanyika Nigeria walikuwa ni timu ya Tanzania ya wasichana na timu ya wavulana ya nchi ya Niger, ambapo wachezaji wote kutoka timu hizo ni miongoni mwa wachezaji 72 wanaofunzwa na makocha wa Manchester United.