Jumatano , 13th Mar , 2024

Nahodha wa Taifa Stars Mbwana Samatta na mlinzi Dickson Job wametemwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ambacho kitaingia kambini Machi 17 kujiandaa na michezo miwili ya kirafiki ya FIFA Series 2024 dhidi ya Bulgaria na Mongolia mnamo Machi 22 na 25-2024.

Akitangaza kikosi hicho mbele ya waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars Hemed Suleiman Morocco ametangaza kikosi cha wachezaji 23 huku ameweka wazi kuwa kikosi hicho ni mchanganyiko wa wachezaji vijana na wenye uzoefu kwa ajili yakutengeneza muunganiko mzuri ndani ya timu hiyo.

“Tutakuwa na mechi mbili za kirafiki tutacheza Machi 22 na 25, mwaka huu dhidi ya Bulgaria na Mongolia, baada ya hapo wachezaji watarejea haraka kwa ajili ya majukumu mengine’’amesema Morrocco.

Kwa upande mwingine,Morocco amesema kupata michezo ya kirafiki na timu kama  Bulgaria ni kitendo kizuri kwani Taifa Stars inapaswa kupata michezo mikubwa ili wachezaji wa timu hiyo wazidi kuwa wakubwa na kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali ambayo kikosi hicho kinashiriki.