Jumatano , 12th Sep , 2018

Nyota wa Tanzania anayekipiga kwenye klabu ya soka ya KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta, amesema amejiongezea ndoto nyingine kwenye maisha yake ambayo ni kumiliki ndege binafsi.

Mbwana Samatta

Samatta amebainisha hilo leo kupitia mitandao yake ya kijamii, baada ya kuweka picha aliyopiga akiwa eneo la Waterschei, Limburg nchini Ubelgiji ambapo nyuma ya picha inaonekana ndege yenye nembo ya klabu yake ya KRC Genk.

Samatta amerejea nchini Ubelgiji akitokea hapa nchini Tanzania, ambapo Jumamosi ya Septemba 8, 2018 aliiongoza timu ya taifa (Taifa Stars), kutoka sare na Uganda kwenye mechi ya kundi L ya kuwania kufuzu fainali za AFCON mwaka 2019 nchini Cameroon.

Nahodha huyo wa Stars ameanza vizuri msimu huu ndani ya klabu yake ya Genk, akifanikiwa kufunga mabao 9 katika mechi 6. Alipiga hatrick kwenye ushindi wa 5-2 dhidi ya Brøndby IF na marudio akafunga goli 1 hivyo kukamilisha bao 4.

Pia alifunga bao 2 dhidi ya Charleroi kwenye mechi ya ligi kabla ya kufunga goli 1 dhidi ya Waasland Beveren, hakuishia hapo akafunga bao 1 kwenye mechi na Zulte Waregem kisha akahitimisha na bao 1 dhidi ya Lech Poznan.