Cristiano Ronaldo akiwa na tuzo yake
Ronaldo ametwaa tuzo hiyo akiwabwaga wenzake Gareth Bale wa Real Madrid pia na Antoine Griezmann w Atletico Madrid waliofikia hatua ya tatu bora.
Kwa mujibu wa kura 55 zilizopigwa, Ronaldo amepata kura 40, akifuatiwa na mfaransa Antoine Griezmann aliyepata kura 8, huku Gareth Bale raia wa Wales akiambulia kura 7 pekee.
Zoezi la upigaji kura liliwashirikisha waandishi 55 wa habari za michezo kutoka nchi wanachama wa UEFA.
Baadhi ya mambo yalichongia Ronaldo kupata tuzo hii ni pamoja na ubingwa wa michuano ya Ulaya kwa ngazi ya vilabu ambapo aliiongoza Real Madrid kutwaa kombe la Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League) kwa msimu huo, kabla ya kuiongoza timu yake ya Taifa ya Ureno kutwaa kombe la Mataifa ya Ulaya UEFA EURO 2016.
Katika msimu huo, Ronaldo amecheza mechi 36 za ligi ya Hispania (La Liga), na kufunga magoli 35 huku akisaidia (assist) magoli 11.
Katika michuano ya Mabingwa Ulaya amecheza mechi 12, akifunga magoli 16 na kusaidia magoli 4.
Katika michuano ya Mataifa Ulaya (UEFA EURO 2016) amecheza mechi 7 na kufunga magoli matatu huku akisaidia magoli matatu.
Hii ni mara ya pili kwa Ronaldo mwenye umri wa miaka 31 kutwaa tuzo hiyo baada ya kufanya hivyo katika msimu wa 2013/14.