Jumatano , 15th Jun , 2022

Taarifa kutoa nchini Ureno zinaeleza kuwa Cristiano Ronaldo sasa atalazimika kulipa pauni milioni 17 za England sawa na Bilioni 47 na zaidi ya Milioni 889 za Kitanzania kwa ajili ya kujenga nyumba yake mpya huko 'Riviera' nchini Ureno ili aishi akistaafu soka.

Cristiano Ronaldo na baadhi ya nyumba anazomiliki hadi sasa.

Mshambuliaji huyo wa Manchester United mwenye umri wa miaka 37, alinunua eneo kubwa sana Quinta da Marinha, kwenye pwani ya magharibi ya nchi yake ya Ureno mapema mwezi september mwaka jana, iliyopewa jina la utani la Mto wa Kireno ('Portuguese Riviera') kutokana na hadhi yake likiwa ni eneo la kifahari na la gharama kubwa.

Ripoti za hapo awali zilidokeza kwamba Ronaldo amepanga kuishi hapo na familia yake wakati atakapo tundika daluga. Nyota huyo wa mashetani wekundu pia anamiliki mali ikiwa ni pamoja na jengo la ghorofa saba huko Funchal mjini Madeira, ambako mama yake Dolores mwenye umri wa miaka 66 na kaka yake Hugo wanaishi baada ya kuinunua miaka miwili iliyopita.

Ronaldo, pamoja na mpenzi wake Georgina Rodriguez na watoto wake wanne, pia ana miliki nyumba ya kifahari mjini Turin nchini Italia aliyonunua wakati akiwa Juventus, pamoja na jumba la kifahari kwenye ngome iitwayo La Finca karibu na Madrid nchini Hispania.

Mpango huu wa kujenga nyumba mpya ni mali iliyopangwa kuongezwa hivi punde ingawa Ronaldo bado hajaonyesha kuwa tayari kustaafu kwa sasa, licha ya ujenzi huo kutarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka ujao.