Jumatano , 13th Oct , 2021

Mshambuliaji hatari wa Klabu ya Azam Fc, Prince Dube atakosa mechi ya hatua ya pili ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids ya Misri itakayochezwa Oktoba 16,2021 saa 9 alasiri katika uwanja wa Azam Complex.

Mshambuliaji wa Azam Fc, Prince Dube akiwa mazoezini

Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Habari na mawasiliano wa Azam Fc, Zacharia Thabit amesema Dube ndiye nyota pekee atakayekosekana katika mchezo huo  lakini wote waliosalia wapo katika hali nzuri.

Dube ambaye msimu uliopita alifunga bao 14 licha ya kucheza michezo michache kufuatia kuandamwa na majeraha, ameanza mazoezi mepesi baada ya kupatiwa matibabu ya majeraha aliyoyapata katika maandalizi ya msimu.

Vilevile Zaka Zakazi amesema kuwa wapinzani wapo, Klabu ya Pyramids inatarajiwa kuwasili nchini saa tatu usiku  na watafanya mazoezi katika uwanja wa Azam Complex.

Azam , Biashara na Simba ndizo klabu zilizosalia katika michuano ya kimataifa zikiiwakilisha Tanzania baada ya Yanga kutupwa nje mapema na Rivers United ya Nigeria.