Alhamisi , 1st Jul , 2021

Timu ya Phoenix Suns imetwaa ubingwa wa ligi ya kikapu nchini Marekani 'NBA' Ukanda wa Magharibi baada ya kuifunga timu ya Los Angeles Clippers kwa alama 130-103 na kufikisha ushindi wa michezo 4-2 katika michezo sita ya mizunguko ya fainali hiyo.

Timu ya Phoenix Suns ikiwa inashangilia ushindi wa kombe la NBA ukanda wa Magharibi baada ya kuifunga Los Angeles Clippers kwa jumla ya michezo 4-2.

Ushindi huo unawafanya Suns kutinga fainali kuu ya NBA inayohusisha mabingwa wa kanda zote mbili ikiwa ni kwa mara ya kwanza tokea mwaka 1993, lakini pia wametwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza baada ya kufeli kucheza hata michezo ya mtoano 'NBA Playoffs' kwa misimu 10 mfululizo.

Phoenix Suns itacheza fainali hiyo na mshindi kati ya timu ya Milwaukee Bucks na Atlanta Hawks ambao kwasasa wamecheza michezo minne wakiwa sare ya ushindi wa michezo 2-2 huku wakitaraji kushuka tena dimbani saa 9:30 usiku wa kuamkia kesho kwa saa za Afrika Mashariki.

Ushindi wa Suns umechagizwa na kiwango bora cha nyota wake, Chris Paul ambaye ni mchezaji wa zamani wa Clippers miaka ya 2011 na 2017, aliyejikusanyia alama 41, rebaundi 4 na assit 8 zilizosaidia kuibeba Suns kwenye mabega yake.

Kwa upande mwingine, assist 8 alizotoa Chris zimefanya afikishe jumla ya assist 1,022 na kushika nafasi ya 11 kwenye orodha ya wache kikapu wenye assist nyingi kwenye historia ya NBA huku akiwa nyuma kwa assist 18 na gwiji wa kikapu, Kobe Bryant mwenye jumla ya assist 1,040 na kushika nafasi ya 10.