Ijumaa , 17th Jun , 2016

Mshauri wa Timu ya Taifa ya vijana ya Tanzania Serengeti Boys Kim Poulsen amewataka wachezaji wa kikosi hicho kupata ushindi wa mapema dhidi ya timu ya vijana ya Shelisheli.

Mshauri wa Timu ya Serengeti Boys, Kim Poulsen akitoa maelekezo kwa vijana katika mazoezi Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.

Poulsen amesema, wachezaji hao wanatakiwa kujijengea mazingira ya kupata ushindi mapema zaidi kwakuwa mchezo huo ni muhimu na Serengeti hawatakiwi kuwadharau wapinzani wao kwani katika soka lolote linaweza kutokea.

Poulsen amesema, ameridhishwa na maandalizi yanayoendelea kwa timu hiyo kwani inaonyesha nia ya kuweza kufanya vizuri katika mchezo wa awali na hata wa marudiano.

Serengeti Boys itavaana na Shelisheli Juni 25 mwaka huu jijini Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa kuwania kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana zinazotarajiwa kufanyika mwakani nchini Madagascar.